MAMBO SITA YA KUZINGATIA ILI UISHI VIZURI NA MKWE WAKO
Maranyingi imekuwa ni tatizo kwa mtu na mkwe wake (hasa mke na mama mkwe) kuishi kwa umoja na upendo. Utakuta mama anaona ni vigumu kuacha mtoto wake wa kiume apangiwe mambo yake na mtu mwingine(mkewe) na mke naye anaona tabu kuchanganyika na familia ya mume. Tatizo hili linaweza kuwa kubwa hata kuhatarisha ndoa na familia. Uelewano na hekima inahitajika sana kutatua matatizo haya.
Hapa nimefafanua baadhi ya mambo machache yanayoweza kukusaidia kuboresha mahusiano yenu.
1. Onyesha upendo kwa vitendo
Usiruhusu kuongozwa na hisia zako, bali umruhusu Mungu akuongoze ili uweze kutenda kwa upendo. Haijalishi unajisikia vipi, chagua kutenda matendo ya upendo kwa mkwe wako (mama au mtoto). Amini kwamba unapoonyesha upendo Mungu atakufungua moyo wako na kukuwezesha kujisikia vyema.
2. Uwe mvumilivu
Usiwe na mategemeo makubwa kuwa siku ya kwanza tu kuonana basi mtapendana na kuwa na mahusiano ya karibu. Jipe mda na pia mpe na yeye muda kwa kuishi kwa kuvumiliana na hatimaye mahusiano yetu yatakuwa na kuimarika. usijaribu kumlinganisha na mama/mtoto wako bali umkubali kwa jinsi alivyo. Pia jaribu kuishi vile ulivyo na usijaribu kuwa mtu mwingine ili kumpendeza mkwe wako.
3. Heshima
Wewe kama ni mke hakikisha unamuheshimu mkwe wako kama mzazi wako na wewe mama kumbuka kuwa mtoto wako ameshakuwa sasa na mkewe ni sehemu yake hivyo heshimu maamuzi yao na uhuru wao. Usiingilie kila kitu wanachokifanya bali subiri hadi pale watakapokuomba ushauri.
4. Tatueni Migogoro
Msiache uchungu na maumivu yakaweka ukuta kati yenu sababu ya kutokutatuliwa. Kama kuna mmoja amemjeruhi mwingine (mara nyingi huwa ni kwa bahati mbaya), hakikisheni kuwa mnatatua jambo hilo mapema na kwa upendo. Uwe tayari kukiri kosa pale unapokuwa umekosea na pia uwe ni mtu wa msamaha. Kama kuna mmoja anaonyesha hataki kubadilika, muombee na uwe naye kwa akili na sio kubishana naye.
5. Weka Mipaka
Lazima kuwe na mpaka ili kila mmoja ajue anatakiwa kufanya nini na kwa kiasi gani. Muwe mmekubalia jinsi ya kukabili mambo fulani ya kifamilia na kwa mipaka gani ili asiwepo wa kufanya asivyotakiwa na kuleta kutokuelewana.
6. Jenga Daraja Kati Yenu
Badala ya kuhukumiana kutokana na tofauti zenu, Jishushe na ufahamu kuwa kuna mengi ya kufundishana kutokana na tamaduni na desturi zenu mbalimbali. Jitahidi kujifunza toka kwake kadiri inavyowezekana na muombe Mungu akuwezesha kumkubali jinsi alivyo. Muonyeshe upendo na kumthamini kwa dhati.
MAMBO SITA YA KUZINGATIA ILI UISHI VIZURI NA MKWE WAKO
Reviewed by
Admin
on
10:15 PM
Rating:
5
No comments:
Post a Comment